Hii ni Kwaresma;
Jumanne asubuhi tarehe 31.03.2026
Marko 11:1-10
1 Hata walipokaribia Yerusalemu karibu na Bethfage na Bethania, kukabili mlima wa Mizeituni, aliwatuma wawili katika wanafunzi wake,
2 akawaambia, Nendeni mpaka kile kijiji kinachowakabili; na katika kuingia ndani yake, mara mtaona mwana-punda amefungwa, asiyepandwa na mtu bado; mfungueni, kamleteni.
3 Na mtu akiwaambia, Mbona mnafanya hivi? Semeni, Bwana anamhitaji na mara atamrudisha tena hapa.
4 Wakaenda zao, wakamwona mwana-punda amefungwa penye mlango, nje katika njia kuu, wakamfungua.
5 Baadhi ya watu waliosimama huko wakawaambia, Mnafanya nini kumfungua mwana-punda?
6 Wakawaambia kama Yesu alivyowaagiza, nao wakawaruhusu.
7 Wakamletea Yesu yule mwana-punda, wakatandika mavazi yao juu yake; akaketi juu yake.
8 Watu wengi wakatandaza mavazi yao njiani, na wengine matawi waliyoyakata mashambani.
9 Nao watu waliotangulia na wale waliofuata wakapaza sauti, Hosana; ndiye mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana;
10 umebarikiwa na ufalme ujao, wa baba yetu Daudi. Hosana juu mbinguni.
Ndiye mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana;
Ni tukio la Yesu kuingia Yerusalemu kwa shangwe ambalo linaandikwa na Injili zote. Injili zinazofanana huandika kuanzia Yesu alivyowatuma wanafunzi wake kumletea mwana punda, Yohana yeye hahangaiki na Yesu alivyoagiza mwana punda, anaandika Yesu akiingia Yerusalemu kwa shangwe. Yesu alipanda mwana-punda, watu wakatandaza nguo zao apite wakiimba Hosana ndiye mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.
Wakati walioimba waliwaza ukombozi toka mikononi mwa utawala wa Warumi, Yesu alikuwa anaiendea njia ya mateso kwa ajili yao na wengine wote. Tumkaribishe aingie mioyoni mwetu, ili kwa njia ya kufa na kufufuka kwake tuurithi uzima wa milele. Amina
Siku njema
Heri Buberwa
