Hii ni Pentekoste;
Jumatano asubuhi tarehe 27.05.2026
Yoeli 2:28-32
28 Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono;
29 tena juu ya watumishi wenu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile, nitamimina roho yangu.
30 Nami nitaonyesha mambo ya ajabu katika mbingu na katika dunia, damu, na moto, na minara ya moshi.
31 Jua litageuzwa kuwa giza, na mwezi kuwa damu, kabla haijaja hiyo siku ya Bwana iliyo kuu na itishayo.
32 Na itakuwa ya kwamba mtu awaye yote atakayeliita jina la Bwana ataponywa; kwa kuwa katika mlima Sayuni na katika Yerusalemu watakuwako watu watakaookoka, kama Bwana alivyosema; na katika mabaki, hao awaitao Bwana.
Roho Mtakatifu ni nguvu yetu;
Agano la kale linaonyesha kuwa Pentekoste ilikuwa mojawapo ya sikukuu ya Wayahudi, ila tu hawakuiita Pentekoste. Wayahudi waliiita sherehe ya mavuno. Inatajwa katika sehemu tano katika Historia;
Kutoka 23
Kutoka 24
Mambo ya Walawi 16
Hesabu 28
Torati 16
Ilikuwa sherehe ya mwanzo wa Juma la mavuno. Pentekoste ilikuwa sherehe ya mwanzo wa mavuno ya ngano. Kwa maana ya Pentekoste iliangukia mwezi wa tano au mapema mwezi wa sita.
Kulikuwa na tamasha, maadhimisho na maandalizi yaliyofanyika kabla ya Pentekoste. Kulikuwa na Pasaka, kulikuwa na mikate isiyotiwa chachu, kulikuwa na sikukuu ya mavuno ya kwanza. Sikukuu ya mavuno ya kwanza ilikuwa sherehe ya mwanzo wa mavuno ya shayiri. Hiyo ndiyo namna siku ya Pentekoste ilivyopatikana. Kwa mujibu wa Agano la kale, ungechukua siku ya mwanzo kabisa ya mavuno ya kwanza, na kuhesabu siku hamsini, ndiyo Pentekoste. Hivyo mazao ya kwanza ni mwanzo wa mavuno ya shayiri, na Pentekoste ni sherehe ya mwanzo wa mavuno ya ngano. Ilikuwa siku ya hamsini baada ya mavuno ya mwanzo, sawa na majuma saba, hivyo kuitwa sherehe ya mavuno, au sherehe ya majuma.
Yajue mambo matatu katika ili uielewe Pentekoste kama inavyoandikwa kwenye Mdo 2;
a) Pentekoste ilikuwa sherehe ya hija.
Kwa sheria ya Kiyahudi, watu wazima wote kutoka sehemu zote walizoishi walienda Yerusalemu ili kuhudhuria tukio hili.
b) Pentekoste ilikuwa sikukuu .
Hakuna huduma yoyote ingepatikana. Huduma zote kama shule, maduka zilifungwa.
c) Kulikuwa na sherehe, yenye sadaka na dhabihu kwa mujibu wa siku hii.
Siku ya Pentekoste, Kuhani alitoa mikate miwili iliyotengenezwa kwa ngano mbele za Bwana. Mikate ilitengenezwa kwa ngano iliyotokana na mavuno ya wakati huo
Kwa ufupi;
Pentekoste wakati wa mitume ilikuwa sherehe kubwa sana ya mavuno. Mitaa ya Yerusalemu ilijaa maelfu ya mahujaji waliotoka sehemu zote kusherehekea uzuri wa Mungu, na shukrani kwa ajili ya mavuno.
Kwa nini Pentekoste ni muhimu kwa wakristo?
Leo hii Pentekoste inaonekana kama sikukuu na sio kusherehekea mavuno. Lakini kukumbuka Roho Mtakatifu alivyolishukia Kanisa (Mdo 2). Siku ile Roho Mtakatifu alilijaza Kanisa nguvu, wakaongezeka waamini 3000 wapya.
Matendo ya Mitume 2:41
[41]Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu.
Yesu alikuwa ameahidi;
Yohana 14:26
[26]Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.
Tukirudi kwenye somo la leo;
Wakati wa Yoeli, watu walikuwa katika mahitaji makubwa. Ukisoma kuanzia sura ya kwanza, utaona wana wa Israeli walivamiwa na nzige. Huu ni wakati ambao watu wa Mungu walikuwa wamerejea Yerusalemu kutoka uhamishoni. Vizazi vya nyuma hawakuwapo tena, lakini wengine walikuwa wamerudi wakijaribu kujijenga upya kimaisha. Kwa waliotegemea ardhi kwa kila kitu katika maisha yao, ikiwemo kutoa sadaka, ilikuwa vizuri sana kwao.
Nzige walikuwa wamekula kila kitu;
Yoeli 1:4-7
[4]Yaliyosazwa na tunutu yameliwa na nzige; na yaliyosazwa na nzige yameliwa na parare; na yaliyosazwa na parare yameliwa na madumadu.
[5]Levukeni, enyi walevi, mkalie;
Pigeni yowe, ninyi nyote mnywao divai;
Kwa sababu ya divai mpya;
Maana umekatiliwa mbali na vinywa vyenu.
[6]Maana taifa limepanda juu ya nchi yangu,
Lenye nguvu, tena halina hesabu;
Meno yake ni kama meno ya simba,
Naye ana magego ya simba mkubwa.
[7]Ameuharibu mzabibu wangu; ameuvunja mtini wangu; ameyaambua magamba yake kabisa; ameuangusha chini; matawi yake yamefanywa kuwa meupe.
Kwa hatua hii tunaweza kusema, hitaji kubwa la mwanadamu yeyote ni kuishi akiwa hai na kupata mahitaji yote muhimu. Nabii Yoeli anaonyesha kuwa watu walikuwa na shida kubwa, kuliko hata hilo janga la kitaifa. Tatizo lao ni kuwa walikuwa wameridhika mno, na kuridhika kwao kulisababisha wasiwe watii kwa Mungu. Yoeli anawaasa kuamka! Watu walikuwa wamekata tamaa kwa Mungu aliyewarudisha katika ardhi yao. Walikuwa kama walevi, na walitakiwa kuona aibu, wakimlilia Mungu.
Mbaya zaidi, Yoeli anasema kwa sababu ya kuridhika kwao, nzige hawakutokea kwa ajali, walitumwa na Mungu;
Yoeli 2:3-4,11
[3]Moto unakula mbele yao; na nyuma yao miali ya moto inateketeza; hiyo nchi inafanana na bustani ya Adeni mbele yao, na nyuma yao imekuwa jangwa tupu; naam, hakuna aliyeokoka asipatikane nao.
[4]Kuonekana kwao ni kama kuonekana kwa farasi; na kama wapanda farasi ndivyo wanavyopiga mbio.
[11]naye BWANA anatoa sauti yake mbele ya jeshi lake; maana matuo yake ni makubwa sana; kwa maana yeye ni hodari atekelezaye neno lake; kwa kuwa siku ya BWANA ni kuu, yenye kitisho sana; naye ni nani awezaye kuistahimili?
Mungu analeta nzige kula mazao, anawaadhibu.
Nini lilikuwa hitaji lao kubwa? Haikuwa ardhi yao, chakula, wala mvinyo! Hitaji lao kubwa lilikuwa kurudisha uhusiano wao na Mungu.
Yoeli 2:12-13
[12]Lakini hata sasa, asema BWANA, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuombolea;
[13]rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie BWANA, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya.
Nabii Yoeli alitaka wajue, na anataka tujue kuwa;
1. Hitaji kubwa la mtu yeyote ni kuwa na uhusiano na Mungu.
Kama ni msomaji mzuri wa Agano la kale, utakumbuka kuwa Mungu na watu wake wako katika Agano la mahusiano. Ukitaka kulijua hili, fikiria mzazi na watoto wake, kama ambavyo baba huwapatia alivyo navyo watoto wake, muda wote, nguvu zote, ulinzi, faraja n.k
Vile vile, na zaidi, Mungu anawajali watu wake;
Kutoka 6:7
[7]nami nitawatwaeni kuwa watu wangu, nitakuwa Mungu kwenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ni YEHOVA, Mungu wenu, niwatoaye mtoke chini ya mizigo ya Wamisri.
Mungu anajua watu wake wanahitaji nini, wanamhitaji yeye.
Tunafikiria hitaji letu kubwa ni nini? Maisha bora? Ndiyo. Lakini zaidi ya yote, tunamhitaji Mungu.
Tukirudi kwenye somo la leo, angalia Mungu anachoahidi kwa watu wake wanaporudi kwa toba na kurudisha uhusiano na Mungu wao.
Yoeli 2:24-27
[24]Na sakafu za kupepetea zitajaa ngano, na mashinikizo yatafurika kwa divai na mafuta.
[25]Nami nitawarudishia hiyo miaka iliyoliwa na nzige, na parare, na madumadu, na tunutu, jeshi langu kubwa nililotuma kati yenu.
[26]Nanyi mtakula chakula tele na kushiba, na kulihimidi jina la BWANA, Mungu wenu, aliyewatendea mambo ya ajabu; na watu wangu hawatatahayari kamwe.
[27]Nanyi mtajua ya kuwa mimi ni katikati ya Israeli, na ya kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu, wala hakuna mwingine; na watu wangu hawatatahayari kamwe.
Mungu anarudisha kila kitu kilichochukuliwa na kuliwa na nzige, na ziada, na kushiba.
Cha kushangaza, pamoja na watu wa Mungu kuasi, Mungu anaahidi kuwa kati ya watu wake. Hakuna kitu unachohitaji, asema Bwana, unamhitaji yeye tu! Ni katika hali hii ya Mungu kubariki watu wake, tunalipata somo la leo.
Yoeli 2:28-32
[28]Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono;
[29]tena juu ya watumishi wenu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile, nitamimina roho yangu.
[30]Nami nitaonyesha mambo ya ajabu katika mbingu na katika dunia, damu, na moto, na minara ya moshi.
[31]Jua litageuzwa kuwa giza, na mwezi kuwa damu, kabla haijaja hiyo siku ya BWANA iliyo kuu na itishayo.
[32]Na itakuwa ya kwamba mtu awaye yote atakayeliita jina la BWANA ataponywa; kwa kuwa katika mlima Sayuni na katika Yerusalemu watakuwako watu watakaookoka, kama BWANA alivyosema; na katika mabaki, hao awaitao BWANA.
Hebu kumbuka siku ulipokuwa unasubiri jambo, kama zawadi ya siku ya kuzaliwa, au mapumziko, au kitu chochote kizuri ukipendacho, na unasubiria kwa hamu. Hebu kumbuka....
Leo tunaisherehekea Pentekoste. Sijui ni kwa muda gani ulisubiria kitu unachokipenda. Lakini, Israel walisubiria kwa miaka mingi Roho ashuke toka kwa Mungu, tangu Nabii Yoeli alipotabiri. Vizazi vilikuwa vikitaarifiwa, na bado waliendelea kusubiri toka kwa Mungu.
Kwa Wayahudi, lilikuwa jambo kubwa. Ni watu wachache katika Agano la kale walibarikiwa kuwa na Roho wa Mungu ndani yao, watu kama Musa, Samsoni na Daudi. Watu hawa walikuwa viongozi, na matumaini ya Nabii Yoeli wakati ule yalikuwa kwamba wale ambao wangejawa na Roho, wangekuwa viongozi. Hivi ndivyo ilivyokuwa wakati wa Agano la kale.
Hivyo mategemeo yao yalikuwa makubwa. Kwa tukio hili kutokea, Yoeli anasema Mungu angenwaga Roho wake juu ya watu. Watu wangekuwa viongozi na kuwapeleka wengine kwa Mungu. Lakini Mungu hakuwa anaenda kuwapa Roho wake watu wachache kuongoza, alikuwa anakwenda kumpa Roho Mtakatifu kila mmoja aliye wake.
Jumapili ya Pentekoste, tunakumbuka Pentekoste ya kwanza baada ya Yesu kupaa. Tunakumbuka Mungu alipomwaga Roho Mtakatifu, sio kwa wayahudi tu, bali kwa watu wa mataifa yote, wake kwa waume, vijana kwa wazee, huru kwa wafungwa. Habari hii inarejea historia, ikitukimbusha kuwa tunamhitaji Mungu, anbaye anajua mahitaji yetu, mojawapo ikiwa ni Roho Mtakatifu aliyetupa kwa neema.
2. Wanaompokea Roho Mtakatifu wako salama.
Kama umewasoma manabii wadogo, utakuwa umewahi kukutana na neno/andiko kama la mstari wa 31, yaani "Siku ya Bwana"
Angalia mstari wa 31;
Yoeli 2:31
[31]Jua litageuzwa kuwa giza, na mwezi kuwa damu, kabla haijaja hiyo siku ya BWANA iliyo kuu na itishayo.
Neno hili lilitumika sana na manabii. Ilionyesha wakati katika historia, ambapo Bwana angerudi duniani, na kungekuwa na alama kama tetemeko, giza, moshi, na miale ya moto. Hizi ni alama za Agano la kale za utakatifu wa Mungu na ulinzi kwa watu wake, kama moshi pale mlimani, ambapo Mungu alimpa Musa amri.
Mungu ni Mtakatifu, ni tofauti kabisa na wanadamu. Mungu sio mdhambi, ni mkamilifu na upendo kamili. Ndio maana havumilii dhambi. Siku hii ya Bwana bado inakuja, kama tujuavyo, kwenye Agano jipya, Yesu atarudi, na hii itakuwa "Siku ya Bwana"
Hapa namaanisha Mungu yuko njiani. Mungu anakuja kuwahukumu waliomkataa;
Yoeli 3:2
[2]nitakusanya mataifa yote, nami nitawaleta chini katika bonde la Yehoshafati, na huko nitawahukumu kwa ajili ya watu wangu, na kwa ajili ya urithi wangu, Israeli, ambao wamewatawanya kati ya mataifa, na kuigawanya nchi yangu.
Jina Yehoshafati, maana yake ni "Mungu wa hukumu" Hapa ni wazi kuwa Mungu anakuja kuhukumu ulimwengu.
Lakini Mungu hawahukumu waliompokea Roho Mtakatifu, wakaishi naye.
Yoeli 2:32
[32]Na itakuwa ya kwamba mtu awaye yote atakayeliita jina la BWANA ataponywa; kwa kuwa katika mlima Sayuni na katika Yerusalemu watakuwako watu watakaookoka, kama BWANA alivyosema; na katika mabaki, hao awaitao BWANA.
Hatuhitaji kuhangaika, wala hatuhitaji kufanya lolote, tofauti na ahadi ya Baba. Siku ya Pentekoste Petro alisema;
Matendo ya Mitume 2:38
[38]Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
Toba inatutoa dhambini na kuturudisha kwa Yesu. Tukimwanini Yesu, tukampokea Roho Mtakatifu tunakuwa salama. Tuaminio, tunayo ahadi ya wokovu, Yesu akirudi, na siku hii bado tunaisubiria. Atakaporudi ukakutana naye, atakuona kama rafiki yake? au adui yake? Umeliita Jina la Bwana? Uko salama?
3. Wanaoishi na Roho wa Mungu, wanatakiwa kutangaza habari njema.
Nini unapenda kuongelea sana? Nyumba yako? Tamthiliya? Mke wako? Watoto wako? Mpira? n.k
Nabii Yoeli anatutaka tuwe na Roho ya kuwapa wengine habari za ufalme wa Mungu. Hataki tuwe na Imani peke yetu, anataka tuwahubirie wote. Nabii Yoeli anatuita kupeleka ujumbe wa wokovu kama yeye ambavyo hakunyamaza.
Yoeli alikuwa nabii. Hivyo alisikia toka kwa Mungu moja kwa moja (sio kama manabii wa siku hizi). Manabii walikuwa kisemeo cha Mungu katika Agano la kale. Kwa kumpoke Roho Mtakatifu, nasi tunaitwa kuwaambia wengine habari za Yesu Mwokozi, kama ambavyo Mitume walifanya toka siku ya Pentekoste. Kumbuka kuwa, Pentekoste haikuwa mwisho siku ile. Mungu hakumtuma Roho Mtakatifu kwa waliohudhuria Siku ile tu, bali Roho Mtakatifu amekuwepo Siku zote.
Injili ni kwa ajili ya wote, na Mungu anawapa Roho Mtakatifu wote aliowaita.
Tunatangaza habari zake?
Tunamhubiri?
Kama siku ya Bwana inakuja, watu wote wanatakiwa kumgeukia Mungu leo. Maana yake tuhakikishe tunahubiri Injili kwa wote ambao tunajua hawajampokea Yesu. Watajuaje wasipoambiwa? Kumhubiri Kristo ni zawadi uwezayo kutoa kwa sababu inatosheleza mahitaji ya mtu, yaani uhusiano na Mungu wake.
Wamuitao Yesu na kumpokea Roho Mtakatifu, wanampokea Yesu Kristo, wako salama, Yesu akirudi kwa hukumu. Wanaompokea Roho Mtakatifu wanapewa kila kitu wanachohitaji katika kuhubiri Injili.
Tunaitwa kumpokea Roho Mtakatifu, atuongoze katika maisha yetu, tukidumu katika Imani ya kweli, toba na msamaha.
Hii ni Pentekoste
Heri Buberwa Nteboya
Mlutheri
0784 968650
