Date: 
13-06-2026
Reading: 
Mithali 1:7-9

Jumamosi asubuhi 13.06.2026

Mithali 1:7-9

7 Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu.

8 Mwanangu, yasikilize mafundisho ya baba yako, Wala usiiache sheria ya mama yako,

9 Kwa maana hayo yatakuwa kilemba cha neema kichwani pako, Na mikufu shingoni mwako.

Kumtegemea Mungu ni maandalizi ya maisha yajayo;

Jumamosi ya leo tunaamka na mwanzo wa Mithali za Suleimani. Suleimani anasema kumcha Bwana ndicho chanzo cha maarifa, bali wapumbavu hudharau hekima na adabu. Suleimani anawaita wasikilizaji na wasomaji wake kushika mafundisho ya Bwana na kuishika sheria yake. 

Suleimani anasisitiza kukataa vishawishi vya kuingia dhambini;

Mithali 1:10-12

10 Mwanangu, wenye dhambi wakikushawishi, Wewe usikubali.
11 Wakisema, Haya! Njoo pamoja nasi, Na tuvizie ili kumwaga damu; Tumwotee asiye na hatia, bila sababu;
12 Tuwameze hai kama kuzimu, Na wazima, kama wao washukao shimoni.

Asubuhi ya leo Suleimani anatukumbusha kumcha Bwana katika maisha yetu, hicho ndicho chanzo cha maarifa. Anatuhimizia kulishika neno la Mungu na kuikataa dhambi. Hiyo ndiyo njia pekee ya kujiandaa kwa ajili ya maisha yajayo. Amina

Jumamosi njema

 

Heri Buberwa