Date: 
15-06-2026
Reading: 
Mathayo 8:18-22

Jumatatu asubuhi tarehe 15.06.2026

Mathayo 8:18-22

18 Naye Yesu alipoona makutano mengi wakimzunguka, aliamuru kuvuka kwenda ng'ambo.

19 Mwandishi mmoja akamwendea, akamwambia, Mwalimu, nitakufuata ko kote uendako.

20 Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota; lakini Mwana wa Adamu hana pa kulaza kichwa chake.

21 Mwingine katika wanafunzi wake akamwambia, Bwana, nipe ruhusa kwanza, niende nikamzike baba yangu.

22 Lakini Yesu akamwambia, Nifuate; waache wafu wazike wafu wao.

Yesu ni mlango wa kuingia mbinguni;

Somo la leo asubuhi linapatikana pia kwenye Injili ya Luka (Luka 9:57-62) ambapo Yesu anafundisha kuhusu wafaao kuwa wanafunzi wake. Kuna aliyemwambia Yesu nitakufuata kokote utakakokwenda, Yesu akamwambia Mwana wa Adamu hana pa kujilaza kichwa chake. Ukiangalia unaona kama Yesu anasema hana mahali pa kulaza hata kichwa chake. Yesu hapa alikuwa anamwambia huyu ndugu kwamba kumfuata Yesu haikuwa kazi nyepesi.

Mwingine alikuwa tayari kumfuata Yesu lakini akaomba ruhusa kwanza akamzike baba yake. Yesu akamwambia awaache wafu wawazike wafu wao, bali yeye akautangaze ufalme wa Mungu. Haimaanishi usishiriki maziko, bali maisha yetu yasitufanye tumuache Yesu.

Sasa ukisoma katika Injili ya Luka, mwingine alitaka kumfuata Yesu, lakini aliomba ruhusa akawaage ndugu zake. Yesu anamwambia kuwa aliyetia mkono wake kulima akaangalia nyuma hafai kwa ufalme wa Mungu. Hapa Yesu alimaanisha kwamba mtu akiamua kumfuata amfuate kwelikweli, asiangalie nyuma.

Ukiangalia ndugu wote watatu tuliowasoma walitaka kumfuata Yesu, lakini bado kuna mambo walitaka kukamilisha. Mfano huu unatukumbusha kuwa imara katika njia ya ufuasi wetu, na kuwa makini katika njia zetu ili tusimuache Kristo. Tuzingatie maisha yetu kuwa ya kumcha Bwana, na kubaki katika njia yake wakati wote. Tumwamini Yesu aliye mlango wa kuingia mbinguni. Amina

Uwe na wiki njema

Heri Buberwa