Jumatano asubuhi tarehe 17.06.2026
Waefeso 2:1-7
1 Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu;
2 ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi;
3 ambao zamani, sisi sote nasi tulienenda kati yao, katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine.
4 Lakini Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda;
5 hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, tumeokolewa kwa neema.
6 Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu;
7 ili katika zamani zinazokuja audhihirishe wingi wa neema yake upitao kiasi kwa wema wake kwetu sisi katika Kristo Yesu.
Yesu ni mlango wa kuingia mbinguni;
Mtume Paulo anawaandikia watu wa Efeso kuhusu maisha ya zamani. Anasema waliishi maisha ya dhambi kwa kuufuata ulimwengu. Anaendelea kusema kuwa waliishi maisha ya kutimiza tamaa za mwili. Lakini kwa huruma ya Mungu, Paulo anasema wameokolewa kwa neema kwa njia ya Yesu Kristo.
Kama Paulo anavyosema, nasi kwa huruma ya Mungu tumeokolewa kwa neema kwa njia ya Yesu Kristo. Hata pale tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu, alituhuisha mwenyewe na kutufufua pamoja naye. Tukae katika Yesu huyu aliye mlango wa kuingia mbinguni. Amina
Siku njema
Heri Buberwa
