Hii ni Kwaresma;
Jumanne asubuhi tarehe 24.03.2026
2 Wakorintho 5:16-19
16 Hata imekuwa, sisi tangu sasa hatumjui mtu awaye yote kwa jinsi ya mwili. Ingawa sisi tumemtambua Kristo kwa jinsi ya mwili, lakini sasa hatumtambui hivi tena.
17 Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.
18 Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho;
19 yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho.
Kwa Yesu kuna upatanisho wa kweli;
Paulo analiita Kanisa la Korintho kuipokea habari ya upatanisho. Mtume Paulo katika somo la leo tunaona akianza kwa kusema kuwa mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya. Yaani mtu akitubu dhambi akamwamini Yesu anapatanishwa na Mungu. Ukisoma mstari wa 18, 19 na 20, neno upatanisho linatokea mara tano! Paulo hapa alikuwa anaweka msisitizo kwa waumini kufanyika wapya kwa damu ya Yesu.
Mtume Paulo analiita Kanisa la Mungu kubadilika na kuwa wapya katika Kristo. Ukiisoma sura ya tano kuanzia mwanzo, Paulo analeta dhana ya uumbaji mpya. Paulo anarejea historia ya uumbaji tangu kale, yaani Mungu alivyofanya uumbaji na kuiweka dunia. Aliwaumba watu ili wamtumikie. Katika kumtumikia huko ndipo Paulo anajenga dhana ya "uumbaji mpya" ambayo anakuja kuihitimisha akiita "upatanisho". Kwa hiyo Paulo anawaita waamini wa Korintho kumcha Bwana wakiwa ndani ya Kristo, yaani wakiwa wamepatanishwa na Mungu kwa njia ya Yesu Kristo.
Kumbe Paulo analeta ujumbe kwa waaminio kuwa Yesu ametupatanisha na Mungu kwa njia ya kifo chake, hivyo kutuita kudumu katika upatanisho huo. Kama tulivyoona mwanzo, tangu zamani Mungu alitaka watu wote wamche yeye, ndiyo maana alimtuma Yesu Kristo kutupatanisha naye. Sasa leo Mtume Paulo anaelezea kwamba Yesu Kristo ndiye ametupatanisha na Baba. Mstari wa 19 Paulo anasema Mungu alikuwa ndani ya Kristo akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake. Hapa tunapewa nafasi kujihoji kama kweli mioyo imepatanishwa na Mungu, na pia sisi kuwa wapatanishi wa wengine kwa Mungu. Katika kujihoji kama kweli tumepatanishwa na Mungu, na kuwapatanisha wengine, ni muhimu kuzingatia mambo yafuatayo;
1.Lazima tufahamu nini hakijaenda sawa kati ya watu, Mungu na uumbaji. Hatuwezi kujua kama tumepatanishwa na Mungu bila kujua tumesimama wapi katika njia ya imani. Yaani tutafakari njia zetu kama kweli zinampendeza Mungu. Tujiangalie kama tunaishi kwa kadri ya mapenzi ya Mungu. Tukilijua hilo, litatupeleka kubadili njia zetu, ili tukae katika upatanisho kama alivyotupatanisha Kristo, pia tuweze kuwaleta wengine kwa Baba.
2.Tuwapende wenzetu, na siyo kuwahukumu.
Kama tulivyoona, sisi tumepatanishwa na Kristo kwa Baba. Lakini pia tunaalikwa kuwaleta wengine wapatanishwe na Baba. Sasa hatuwezi kuwaleta wengine kwa upatanisho kama hatuwapendi. Hapa ndipo nakumbuka amri kuu ya Upendo katikati ya Kanisa la Mungu. Upendo ukitawala, Kanisa lote litapatanishwa na Mungu.
3.Kama matokeo ya uumbaji wa Mungu, tubaki katika ushirika na Mungu.
Hoja yangu hapa ni kuwa asili ya upatanisho wa mwanadamu kwa Mungu ni Mungu mwenyewe. Somo limetuonesha kuwa Mungu alitupatanisha kwake kwa njia ya Kristo. Hivyo hakuna upatanisho unaoweza kutokea nje ya kuwa na ushirika na Kristo Yesu. Tafsiri yake ni kuwa sisi tuliompokea Yesu tubaki kwake milele, maana ndiko kwenye upatanisho wa kweli.
Heri Buberwa Nteboya
Mlutheri
0784 968650
