Date:
18-05-2026
Reading:
Zaburi 50:15
Jumatatu asubuhi tarehe 18.05.2026;
Zaburi 50:15
Ukaniite siku ya mateso; Nitakuokoa, na wewe utanitukuza.
Mungu utusikie katika kuomba kwetu;
Zaburi ya 50 ni wimbo unaoonesha hukumu ya Mungu kwa watu wake. Zaburi inasisitiza moyo safi na maisha ya utii kuliko kafara za sadaka. Mungu anaonekana kukaa kwenye kiti chake cha enzi kwa hukumu, anaita mbingu na dunia tayari kwa hukumu. Mungu anawaambia Israeli kwamba hana shida na sadaka zao za wanyama, kwa sababu vitu vyote ni mali yake, anaitaka mioyo iliyopondeka.
Mstari wa 15 ambao ndilo somo la asubuhi ya leo, ni sauti ya Mungu akiwaita watu wake kumuita siku ya mateso, anaahidi kuwaokoa, nao wamtukuze. Kwa hiyo kwa mujibu wa Zaburi ya 50, Bwana anawaita watu wake kumcha ili wasiingie hukumuni. Basi tumche Bwana kwa kumtegemea yeye ili tusiingie hukumuni, yaani tuwe na mwisho mwema. Tumuite awe nasi daima, maana yeye husikia kuomba kwetu, ili atutunze na hata kutufikisha kwenye uzima wa milele. Amina
Uwe na wiki njema
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650
