Date: 
28-05-2026
Reading: 
Isaya 44:1-5

Hii ni Pentekoste;

Alhamisi asubuhi tarehe 28.05.2026

Isaya 44:1-5

1 Lakini sikia sasa, Ee Yakobo, mtumishi wangu; na Israeli, niliyekuchagua;

2 Bwana, aliyekufanya, na kukuumba toka tumboni, yeye atakayekusaidia, asema hivi; Usiogope, Ee Yakobo, mtumishi wangu; na wewe, Yeshuruni, niliyekuchagua.

3 Kwa maana nitamimina maji juu yake aliye na kiu, na vijito vya maji juu ya mahali pakavu; nitamwaga roho yangu juu ya wazao wako, na baraka yangu juu yao utakaowazaa;

4 nao watatokea katika manyasi, kama mierebi karibu na mifereji ya maji.

5 Mmoja atasema, Mimi ni wa Bwana; na mwingine atajiita kwa jina la Yakobo; na mwingine ataandika juu ya mkono wake, Kwa Bwana, na kujiita kwa jina la Israeli.

Roho Mtakatifu ni nguvu yetu;

Somo la leo linaangukia sehemu ya pili ya kitabu cha Isaya ambapo wana wa Israeli walikuwa uhamishoni. Maudhui ya somo la leo ni ahadi ya baraka za Mungu kwao wana wa Israeli, kwamba ipo siku hali ya maisha yao itabadilika, yaani kutoka uhamishoni walipokuwa. Baraka inatamkwa katika mstari wa 3 inayohusu kumimina maji mahali pakavu, lakini kumwaga Roho wa Bwana kwa uzao wote wa Israeli. Kumwaga Roho kwa watu wake (Bwana) kunaonekana sawa na kumwaga baraka katika somo. Yaani mstari wa 3 unaandikwa hivi;

-nitaminina maji...

-nitamwaga roho...

-na baraka yangu juu yao...

Uandishi wa Isaya unatumia picha ya mvua kunyesha sehemu kavu, pasipo maji kabisa. Kumbe ni Mungu anaahidi kuwarejesha watu wake kwenye nchi yao. Hii ni picha ya Roho Mtakatifu kuwa kwa watu wa Mungu, ahadi itokayo kwa Mungu mwenyewe.

Mstari wa 4 unaiendeleza lugha ya picha inayotumiwa na Isaya, kwamba Roho akimwagwa wazao wote watatokea kama nyasi, kama mimea karibu na mifereji ya maji. Hapa ahadi ya Mungu ilikuwa kuwabariki watu wake, na wachanue kama mimea ikuayo haraka kwa uzuri kwa kupata maji baada ya ukame. Mimea iliyokauka itaota kwa upya (4), hapa Isaya anaonesha ambavyo watu wenye dhambi wanaahidiwa kusamehewa na kurejea kwa Bwana kwa upya. Mstari wa 5 unaonesha matokeo ya waliookolewa, watajiita Bwana, mwingine kwa jina la Yakobo. Hawa watakuwa wana wa Mungu, yaani jamii ya watu wa Mungu waliookolewa. Kujiita "wa Bwana", "Yakobo" ni kutangaza ushindi wa Bwana aliyewaokoa. 

Isaya anaonesha jinsi ambavyo wakristo wanatakiwa kuwa, anatabiri jinsi ambavyo Yesu angekuja na kuibariki dunia kwa kufa msalabani na kufufuka. Yesu alipaa mbinguni (tuliona siku ya kupaa kwa Yesu Kristo) kwa Baba na kumtuma Roho Mtakatifu kuwa juu ya wote wenye mwili (Mdo 2:17-21, 32-33). Kuna jambo la muhimu hapa, kwamba kwa somo tulilosoma Isaya alikuwa anaongea na watu hawa hapa;

Isaya 43:22-23

22 Lakini hukuniita, Ee Yakobo, bali umechoka nami, Ee Israeli.
23 Hukuniletea wana-kondoo kuwa kafara zako, wala hukuniheshimu kwa dhabihu zako. Sikukutumikisha kwa matoleo, wala sikukuchosha kwa ubani.

Isaya alikuwa anaongea na watu tunaowaona hapo juu, kwamba walikuwa utumwani, walikuwa wamechoka na Bwana, hawakutoa dhabihu, yaani hawakumcha Bwana. Lakini kwa somo la leo, Isaya alitabiri watu wa leo, ambao tunawasoma katika mstari wa 4 na 5 (soma tena hapo juu mwanzo kabisa). Isaya anatabiri watu ambao watampokea Roho Mtakatifu na kuenenda wakimcha Bwana katika maisha yao. Kwa hiyo Isaya anaongelea maisha yetu leo, kwamba Roho Mtakatifu ni Mungu mwenyewe atutakasaye. Kumbe Roho Mtakatifu yupo kwa ajili ya wote, siyo kwa baadhi wajifanyao kummiliki. Nguvu ya Roho Mtakatifu iko kwa kila aaminiye ikimsaidia kushinda majaribu, ndicho Isaya anachoandika. Mungu wetu aweza kutuepucha na ukame, yaani mioyo iliyovunjika na kutuhuisha katika utukufu wake. Kumwagwa kwa Roho Mtakatifu kwa Kanisa la Mungu ni tangazo la Mungu kuwa na watu wake daima.

Roho Mtakatifu ni nguvu yetu;

Alhamisi ya leo tunaendelea na kumbukumbuya Pentekoste. Ni kumbukumbu ya Roho Mtakatifu kuwashukia Mitume, ni siku Kanisa lilianzishwa. Siku ile watu walikuwa wamekaa, mara ghafla uvumi ukatokea, Mitume wakaanza kunena kwa lugha, na kundi lililokuwepo likawasikia watu wakinena kwa lugha zao wenyewe! Hii ilikuwa ajabu kwa waliokuwepo! (Soma Matendo ya Mitume 2). Siku hizi watu wanakushanyika uwanjani wanaambiwa anza kunena. Wengine wanaambiwa sema ahsante Yesu...ahsante Yesu...wanarudia mara nyingi, tayari kunena kwa lugha. Ni wazi kwamba neno lolote ukilirudia mara nyingi kwa haraka utaanza kuongea maneno yasiyoeleweka! Hayo ni mafundisho ya kitapeli, ambayo hayawasaidii waamini kwa lolote, wizi mtupu! Na wengine leo wapo wanaoadhimisha Pentekoste kwa njia hiyo! Kwamba Roho Mtakatifu ni kunena kwa lugha? Kunena kwa lugha ni karama kweli, lakini kwa utaratibu, na siyo huo utapeli.

Isaya leo ameweka vizuri kuhusu Roho Mtakatifu, kwamba Mungu alitoa ahadi ya baraka kwa Taifa lake. Katika ahadi hiyo yumo Roho Mtakatifu, ambaye aliwashukia Mitume. Ifahamike, Roho Mtakatifu ni Mungu mwenyewe, hayuko mifukoni mwa baadhi ya walimu wa neno (matapeli) wanaomhubiri Roho Mtakatifu wakisema pokeaaaaa! Roho Mtakatifu yuko ndani mwetu, hutuongoza daima. Mawazo, maneno na matendo yetu yanaongozwa na Roho Mtakatifu, pale tunapokaa kwa Kristo. Isaya ametoa picha ya mimea kuchanua upya baada ya kupata maji. Roho Mtakatifu akikaa kwetu na kutuongoza tunashinda, maana yeye ni nguvu yetu. Amina

Alhamisi njema

 

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650 

bernardina.nyamichwo@gmail.com