Date: 
09-06-2026
Reading: 
Kutoka 34:1-9

Jumanne asubuhi tarehe 09.06.2026;

Kutoka 34:1-9

1 Kisha Bwana akamwambia Musa, Chonga mbao mbili za mawe mfano wa zile za kwanza; nami nitaandika juu ya mbao hizo maneno hayo yaliyokuwa juu ya mbao za kwanza, hizo ulizozivunja.

2 Nawe uwe tayari asubuhi, na asubuhi ukwee juu katika mlima wa Sinai, nawe hudhurisha nafsi yako kwangu huko katika kilele cha mlima.

3 Asikwee mtu pamoja nawe, wala asionekane mtu awaye yote katika huo mlima; wala kondoo na ng'ombe wasilishe mbele ya huo mlima.

4 Naye akachonga mbao mbili za mawe mfano wa zile za kwanza; na Musa akainuka na mapema asubuhi, naye akakwea katika mlima wa Sinai, kama Bwana alivyomwamuru, akazichukua hizo mbao mbili za mawe mkononi mwake.

5 Bwana akashuka ndani ya lile wingu, akasimama pamoja naye huko, akalitangaza jina la Bwana.

6 Bwana akapita mbele yake, akatangaza, Bwana, Bwana, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli;

7 mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi; wala si mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe; mwenye kuwapatiliza watoto uovu wa baba zao, na wana wa wana wao pia, hata kizazi cha tatu na cha nne.

8 Musa akafanya haraka, akainamisha kichwa chake hata nchi, akasujudu.

9 Akasema, Ikiwa sasa nimepata neema mbele zako, Bwana, nakuomba, Bwana, uende kati yetu, maana ni watu wenye shingo ngumu; ukasamehe uovu wetu na dhambi yetu, ukatutwae tuwe urithi wako.

Kumtegemea Mungu ni maandalizi ya maisha yajayo;

Neno la asubuhi ya leo ni Musa anaagizwa mbao mbili nyingine tena kama zile alizokuwa amezivunja, na Mungu anaahidi kuandika maneno yale yale kama ya mwanzo. Musa anaamriwa kukwea peke yake mlimani. Musa alikwea mlimani, Bwana akamtokea akitangaza kuwa yeye ni mwenye huruma, mwenye rehema, si mwepesi wa hasira, husamehe uovu na dhambi zote. Musa aliinama chini akaomba rehema ya Mungu kwa watu wake maana walikuwa na shingo ngumu, aliomba Mungu akawasamehe. 

Ndivyo Mungu alivyowahudumia watu wake kwa wakati huo. Ulifika wakati akaja kwa njia ya mwili, akafa msalabani, akafufuka na kupaa mbinguni. Huyu ndiye Yesu Kristo ambaye hutusamehe dhambi zetu tunapomwamini na kutubu. Tunayo ahadi ya kusamehewa dhambi na Yesu Kristo, hivyo tumtegemee yeye kwa maandalizi ya maisha yajayo. Amina.

Siku njema

 

Heri Buberwa